بسم الله الرحمن الرحيم

MAJINI

1

Uhakika wa kuwepo kwa majini

 

Sheikh Mustafa Mohamed Kihago

 

HOME

 

MAJINI 1 MAJINI 2 MAJINI 3 MAJINI 4 MAJINI 5 MAJINI 6 MAJINI 7 MAJINI 8 MAJINI 9

 

Bonyeza hapa kusoma maudhui ya kila makala

 

 Shukrani za dhati zimwendee Allah (SWT). Pia rehema na amani ziwe juu ya kipenzi chake Muhammad (SAW), pamoja na Masahaba wake wote.

 

UHAKIKA WA KUWEPO KWA MAJINI

 

Kuna watu waliodai kwamba majini ni ile hali ya shari iliyopo katika nafsi ya mtu, pamoja na ile nguvu ya ubaya iliyopo ndani ya mtu. Wenye imani za maruhani nao pia wanathibitisha kuwepo majini isipokuwa wao wanawaita kwa majina ya roho za ndani. Nao wanadai ya kwamba maruhani hayo yaliyomo ndani ya mtu ni wepesi kuitikia kutokana na udhaifu wao. Ama kwa upande wa maruhani ya nyota si wepesi kuitika isipokua yanasifika kwa nguvu yalizokua nazo. Vile vile washirikina nao wamesema kwamba: Makusudio ya neno jinni ni roho za nyota. Lakini watu wengi waliobaki wanaamini kuwepo ulimwengu wa majini. Ama wale ambao wanaokanusha kuwepo ulimwengu wa majini hutoa ushahidi wao mbali mbali. Lakini msingi mkubwa wa ushahidi wao umesimamia kwamba wao hawafahamu kama kuna ulimwengu huo wa majini. Na ili kuwajibu hawa wanaokanusha kuwepo huo ulimwengu wa majini, ni kuwaambia kwamba, kushindwa kujua kitu kama hakipo si ushahidi wa kutosha wa kulikanusha.

 

Hakuna kutofautiana katika makundi ya kiislamu kuhusu suala la kuwepo majini kwa kauli ya Ibn Taymiyah, wala hakuna tofauti za rai kwamba Allah (SWT) amemtuma Muhammad (SAW) kwa hao majini pia. Kuna dalili chungu nzima zinazothibitisha kuwepo ulimwengu wa majini ambazo zimepokewa kwa ( tawatur ) katika aya za Qur-an na katika hadithi za Mtume (SAW) kuna hadithi nyinginezo zimepatikana kwa kushuhudia kwa macho. Ama kuhusu maandiko ya Qur-an na aya zinazothibitisha kuwepo ulimwengu wa majini ni nyingi, tutazitaja baadhi yake. Neno la Allah (SWT): "Na sikuumba majini na watu isipokua tu waniabudu" na kauli yake isemayo: "Na hakika kulikuwa na wanaume miongoni mwa wanadamu wakijikinga kwa wanaume miongoni mwa majini kwa hiyo wakuwazidishia taklifu ( kama hivi wenye pepo wakataka hao mapepo kuchezewa ngoma na kuchinjiwa wanyama )". Na pia akasema: "Sema nimepewa ufunuo kwamba walisikiliza kundi la majini", "Na majini tumewaumba kabla kutokana na moto wa upepo wenye joto kubwa". Ama kuhusiana na hadithi za Mtume ( S A W) ni nyingi tutataja baadhi tu: Neno lake mtume (SAW): "Majini wapo aina tatu, aina ya mwanzo wanapaa katika hewa, aina ya pili ni majoka na majibwa na aina ya tatu wanadhihiri na kupotea", imepokewa na Hakim, Twabraniy na Bayhaqiy katika mlango wa ( Al-Asmaai was Swifaat ) kwa isnaad sahih.

 

Na kuna hadithi nyinginezo nyingi tu zinazofahamisha ushahidi wa wazi kuhusu kuwepo majini, tutazitaja hapo baadaye. Ama kuhusu walioshuhudia kuwepo majini mfano ni kama alivyosema Al-A'mash - Mwanazuoni mjuzi: "Alitutokea jinni na nikaliambia: 'Ni chakula gani kizuri mno kwenu?' Akajibu jinni huyo: 'Wali.'" Akasema: "Tukawaletea wali, nikawa ninaona tonge likinyanyuliwa bila ya kuona mtu. Nikauliza: 'Je hata ninyi mna tabia hizi za kupenda vitu fulani fulani kama sisi?' Jinni likajibu: 'Ndiyo.' Nikamwuliza: 'Ni nani wapingaji miongoni mwenu?' Likasema: 'Ni wale washari wetu.'" Isnadi ya kisa hiki ni sahihi kutokana na A'mash, kama alivyosema Al-Hafidh Abul-Hajjaj Al.-Mazey.

 

Hivyo basi, kuwepo kwa majini ni jambo lililothibiti kwa "tawatur" ya Qur-an na Sunnah na ushuhuda.

 

Lakini bado anaweza kuuliza muulizaji na akasema: lakini ni nani hao majini ambao mnathibithisha kuwepo kwao?

 

Jibu la swali hilo tutalitoa katika toleo lijalo.

 

WABILLAHI TAWFIQ

و بالله التوفيق