بسم الله الرحمن الرحيم

MAJINI

2

Ni nini Majini, wameumbwa na mada gani, lini wameumbwa, na wako aina ngapi?

 

Sheikh Mustafa Mohamed Kihago

 

HOME

 

MAJINI 1 MAJINI 2 MAJINI 3 MAJINI 4 MAJINI 5 MAJINI 6 MAJINI 7 MAJINI 8 MAJINI 9

 

 Bonyeza hapa kusoma maudhui ya kila makala

 

Tunamshukuru Allah (SWT) na tunamtakia rehema na amani Mtume wetu Muhammad (SAW) na masahaba wake wote.

 

Leo hii tunaendelea na mada yetu ya Ulimwengu wa majini.

 

1. Ni kitu gani majini?

 

Majini ni viumbe miongoni mwa viumbe vya Allah (SWT) wanatofautiana na binadamu na vile vile malaika . Lakini kuna sehemu kadhaa ambapo hushirikiana na binadamu katika sifa, sifa ya uhuru na uwezo wa kuchagua ‘baina ya haki na batili, makosa na usahihi, kheri na shari’. Tofauti iliyopo kati yao na binadamu ni ya kile kinachojulikana kama asili ya maumbile kwani maumbile ya majini yanatofautiana na maumbile ya binadamu.

 

2. Ni mada ipi walioumbiwa nayo majini?

 

Allah (SWT) ametufahamisha ya kuwa amewaumba majini kutokana na moto na hiyo ni katika aya tofauti mfano, Neno lake Allah ( S W T): "Na majini tumewaumba hapo mwanzo kutokana na moto wa upepo wenye joto kubwa", Al- Hajar 27 . Na akasema katika aya nyingine katika sura ya Ar-Rahman, aya ya 15: "Na akaumba majini kutokana na ( ncha ) ya ulimi wa moto".

 

Vilevile Mtume (SAW) ameeleza kuhusu namna walivyoumbwa majini wakati aliposema: "Wameumbwa malaika kutokana na nuru, wakaumbwa majini kutokana na ulimi wa moto. Na wameumbwa binadamu kutokana na namna mlivyoelezwa." Hadithi hii imetolewa na Muslim kutokana na Bi Aisha (RA)

 

Hivyo basi asili ya kuumbwa majini kwa mujibu ya maelezo yaliyomo ndani ya Qur-an na Sunna za Mtume Muhammad (SAW) ni kwamba wameumbwa kwa moto. Hivyo jinni kwa asili yake ni moto. Lakini wameondoka kweye ile asili yao ya moto kama vile mwanadamu asili yake ni udongo, lakini mwanadamu alivyo si udongo, isipokuwa asili tu ndio udongo. Hivyo, majini nao wana asili tu ya moto lakini si moto wenyewe, kwani kuna ushahidi wa hadithi ya Mtume (SAW) ambayo inafahamisha kwamba majini si moto kama tunavyofahamu wa kuunguza isipokuwa ile ilikuwa tu asili ya maumbile yao. Na kuthibitisha kwamba majini hawapo tena katika yale maumbile yao ya asili ( moto ) ni tamko lake Mtume (SAW): "Hakika adui wa Allah (SWT) Ibilisi, alinitokezea na kijinga cha moto ili anichome nacho katika uso wangu." Imepokewa na An-Nasaiy. Vilevile Imam Ahmad amepokea kutokana na Mtume (SAW) kwamba kuna mtu alimuuliza Abdur-Rahman bin Khanbash: “Nini alifanya Mtume (SAW) wakati alipojiwa na mashetani?”. Alisema: “ Mashetani walimjia Mtume (SAW) kutokea majimbo fulani, wakamteremkia kutoka majabalini huku akiwepo Shetani na kijinga cha moto kwa ajili ya kumchoma nacho Mtume (SAW), akasema: 'Alitishika'. Jaabir akasema: 'Nami nilihisi hivyo hivyo ( kwamba .Mtume (SAW) atatishika )'. Akasema:  'Akawa anarudi nyuma'. Akasema: 'Akamtokezea Jibril (AS) akasema: 'Ee Muhammad sema', Mtume (SAW) akauliza,'niseme nini?' Akamwambia, 'Sema: Najilinda kwa maneno ya Allah (SWT) yaliotimia, maneno ambayo hafui dafu yeyote juu ya maneno hayo ikiwa ni mwema, mbaya kutokana na shari ya alichokiumba, na kudhurika na shari ya kinachoteremka kutoka mbinguni na shari ya kinachopanda. Na shari ya fitna za usiku na mchana. Na shari iliyopo ardhini na ile itokayo ardhini, Ee Rahman.' Na hapo ukazimika moto wa mashetani kwa uwezo wa Allah ( S W T)."

 

Hivyo basi tunapata kuelewa kutokana na hadithi hii kwamba lau kama majini wangekuwa wapo katika yale maumbile yao ya asili ( moto ) na kwamba wao wanaunguza, isingehitajika mmoja kati ya hao mashetani kubeba kijinga cha moto. Kwani ingetosha tu kuwa mkono wa shetani au kiungo chake chochote kinatosha kumunguza binadamu kama vile ambavyo mwanadamu huchomwa na moto akiugusa. Hivyo inaonyesha dhahiri kwamba ule moto walioumbiwa Majini umetapakaa katika maeneo yote ya umbile la majini na kuwa ni viumbe ambao hawaunguzi isipokuwa wao pia huungua kwa moto. Na bila shaka yoyote, Majini huwa wanakula na kunywa kama tulivyo sisi. Pia hukua kimaumbile kama akuavyo mwanadamu kwa kula na kunywa. Na katika vyakula vyao kuna ambavyo ni vya baridi na vya moto. Na kutokana na kuzaana kumewageuza wao kutoka kwenye ile mada ya moto walioumbiwa mwanzo na kuwa na sifa nne: (1) Joto (2) Baridi (3) Majimaji (4) Ukavu.

 

3. Ni lini yaliumbwa majini ?

 

Kuna kauli nyingi zinazozungimzia kuhusu hasa ni lini Allah (SWT) aliwaumba Majini, lakini kauli zote hizo hazina ushahidi wa Qur-an au Sunna za Mtume (SAW) hivyo sisi hatutozizungumzia . Hivyo tunaweza tu kusema kwamba, Majini waliumbwa kabla ya kuumbwa mwanadamu na hivyo ni kutokana na kauli yake Allah (SWT) aliposema, "Na tulimuumba mwanadamu kwa udongo mkavu unatoa sauti ( unapogongwa ), unaotokana na matope mepesi meusi yaliyovunda, na majini tuliwaumba kabla , kwa moto wa upepo wenye joto ( kubwa kabisa )", Al - Hijr 26 - 27 . Hivyo ameweka wazi Allah (SWT) katika aya hizi kwamba Majini yaliumbwa kabla ya mwanadamu.

 

4. Ni aina ngapi za majini?

 

Majini yapo aina tatu kama ilivyokuja katika hadithi za Mtume (SAW) ambapo imetajwa na Ibun Aby Dunia katika kitabu cha "Makaidish - Sheitaan" kutokana na Abud - Dardaa, kwamba Mtume (SAW) amesema: "Allah (SWT) amewaumba majini ya aina tatu: Aina ya kwanza ni majoka , nge na wadudu wa ardhini. Aina ya pili ni kama upepo hewani. Na aina ya tatu ni wale watakaohesabiwa kwa mabaya yao na mazuri yao."

 

Ndugu mwislamu mada hii ina makusudio ya kukuelimisha kuhusu mambo ambayo yameelezwa katika Qur-an na Sunna za Mtume Muhammad (SAW) kuhusiana na ulimwengu wa Majini ambao watu wengi hasa sisi waislam hutuujui, na ni vipi mwanadamu anahusika na ulimwengu huu.

 

WABILLAHI TAWFIQ

 

و بالله التوفيق