بسم الله الرحمن الرحيم
MAJINI
4
Je Iblis ni katika Majini au Malaika?
Sheikh Mustafa Mohamed Kihago
MAJINI 1 | MAJINI 2 | MAJINI 3 | MAJINI 4 | MAJINI 5 | MAJINI 6 | MAJINI 7 | MAJINI 8 | MAJINI 9 |
Bonyeza hapa kusoma maudhui ya kila makala
Shukrani za dhati zimwendee Allah (SWT). Pia rehema na amani ziwe juu ya kipenzi chake Muhammad (SAW), pamoja na masahaba wake wote.
Tamko ( Jinni ) limekaririwa katika Qur-an Tukufu mara ishirini na mbili. Hivyo, limetajwa pekee neno ( Jinni ) pasi na kuambatanisha na neno ( Insi ) mwanadamu mara nane katika sehemu tofauti, kuhusiana na kuambatanishwa kwa neno ( Insi ) mwanadamu na neno ( Jinni ) limetajwa mara kumi na tano ndani ya Qur-an Tukufu.
Ndugu mwislam, makala hizi kuhusiana na ulimwengu wa majini ni njia na wala sio lengo. Kama vile ambavyo Qur-an Tukufu inavyozungumzia maswala tofauti yakiwepo yanayohusu visa vya manabii na historia za mitume, Qur-an haikuifanya sura nzima ili iwe tu ni darasa kuhusiana na majini, na ili kujua hali za maisha yao na namna ya sifa zao isipokua lengo na dhumuni hasa la Qur-an kuwekewa sura kama hii ni kuzitia nguvu imani juu ya tawheed ya kuhusu Allah (SWT), pia kuitukuza misingi ya dini ya kiislam kwamba viumbe vya Allah (SWT) ambavyo vilivyoumbwa kwa udongo, na vile vilivyoumbwa kwa nuru na moto, vyovyote vilivyo ikiwa vinaonekana au havionekani, ikiwa ni vizuri au vibaya, vyote vipo chini ya ufalme wa Allah (SWT) mwenye uwezo wa kila kitu. Na kwamba hivyo viumbe vitahesabiwa kutokana na matendo yao.
1. Je Ibilisi ni katika majini au malaikah?
Kuna mawazo tofauti kuhusiana na jambo hili kati ya wanazuoni wa tafsiri. Imam Shahid Sayyid Qutb amesema katika tafsiri yake "Fidhilalil Qur-an" kwamba Iblisi ni katika majini, kwani neno la Allah (SWT) katika suratul Baqarah, aya 34 ," isipokua Iblisi" linafahamisha kwamba alikua si Malaikah isipokuwa yeye alikua pamoja na Malaikah wakati ilipotolewa amri ya kumsujudia Adam (AS).
Kuna rai nyingi nyingine zinazodai kwamba Iblisi ni katika Malaikah, lakini zote hazina nguvu mbele ya neno lake Allah (SWT) aliposema: "isipokuwa Iblisi alikua ni katika majini akaiasi amri ya Mola wake." Al-Kahf 50. Vile vile ushahidi mwingine wa kuthibitisha ya kwamba Iblisi ni katika majini ni neno lake yeye Mwenyewe Iblisi alipokua akizungumza na Allah (SWT) aliposema : "Umeniumba kutokana na moto, na kumwumba yeye ( Adam A S ) kutokana na udongo." Al 'Araf 12.
Na vile vile Iblisi ana watoto kinyume na malaika, na kwamba malaikah wao wapo kama vile walivyoelezea na Allah (SWT): "Hawamwasi Allah katika amri zake na wanatekeleza kila wanaloamrishwa."At-Tahrim 6. Izingatiwe kwamba malaikah wameumbwa kutokana na nuru, lakini majini wameumbwa kutokana na moto. Imepokewa na Aishah (RA) kutoka kwa Mtume (SAW) kwamba amesema : "Wameumbwa Malaikah kutokana na nuru, wakaumbwa majini kutokana na moto, na akaumbwa Adam kutokana na vile mlivyoelezewa." Imepokewa na Muslim. Hivyo basi Iblisi ni katika majini wala si Malaikah.
2. Je Majini wana husdah?
Jawabu ni ndiyo kwani jicho lipo la aina mbili : kuna jicho la kibinadamu, na jicho la kijini. Na imepokewa hadithi sahihi kutokana na Umu Salamah (RA) kwamba Mtume (SAW) alimwona kijakazi huko kwa ( Umu Salama ) akiwa na alama usoni mwake akasema (SAW): "Mfanyeni kisomo kwani yeye amepatwa na kijicho", yaani jicho baya la kijini.
Na imepokewa na Bukhari kutokana na Abu Hurayrah (RA) kwamba Mtume (SAW) amesema: "Kijicho ni kweli kipo, na akakataza kujichora." Rejea mlango wa Tiba katika Sahih Bukhari.
3. Ni vipi anatakiwa mwislam kuamini kuhusiana na majini?
( a ) Wao ( Majini ) ni viumbe wa Allah (SWT), kama ambavyo Allah (SWT) aliumba malaika vile vile aliumba majini na watu
( b ) Qur-an Tukufu haikuelezea namna ya sifa ya ndani ya maisha ya majini isipokua tu vile walivyoumbwa kwa moto, na namna ya kuongea kwao na sisi kuongea nao na kuwasiliana nao
( c ) Lakini la kuzingatia mno ni kwamba Qur-an kwa nguvu zote inakataza watu kutaka msaada kutoka kwa majini au kuwategema, kuwaogopa n.k kwani atakaye wafanya kuwa ni wapenzi wasaidizi, na kuomba kinga kutoka kwao kinyume na Allah (SWT), Allah (SWT) atamdhalilisha huyo atakayefanya hivyo. Kwani majini hawana uhusiano wowote na mwanadamu katika maisha yao. Hawawashi wala hawazimi, wala hawatufanyii lolote gumu kuwa jepesi, wala hawafanyi lililopo mbali kuwa karibu. Wala hawana uwezo wa kumdhuru adui yetu.
Mwisho wa yote wao ( majini ) ni viumbe waliopo chini ya mamlaka ya Allah (SWT) hawatoki kwenye himaya yake, wala hawawezi kutoka nje ya hukumu zake. Ndugu mwislam uislam ni ITIKADI iliyokuwa mbali mno na ushirikina kwa kutapeli watu, kwa kutabiri mambo yatakayotokea kwa uongo.
Usikose toleo lijalo kuhusu majukumu ya majini.
WABILLAHI TAWFIQ
و بالله التوفيق