بسم الله الرحمن الرحيم
MAJINI
6
Maisha ya Majini ya kijamii ( Ndoa zao, ndoa kati ya Majini na watu )
Sheikh Mustafa Mohamed Kihago
MAJINI 1 | MAJINI 2 | MAJINI 3 | MAJINI 4 | MAJINI 5 | MAJINI 6 | MAJINI 7 | MAJINI 8 | MAJINI 9 |
Bonyeza hapa kusoma maudhui ya kila makala
Shukrani za dhati zimwendee Allah (SWT). Pia rehema na amani ziwe juu ya kipenzi chake Muhammad (SAW), pamoja na masahaba wake wote.
Majini nao wana maisha yao ya kijamii, na katika mada hii tutazungumzia dondoo zifuatazo:
( a ) Je majini wanaoana na kuzaliana?
( b ) Je anaweza mwanadamu kuoana na jini na inakuaje?
( c ) Je ndoa kati ya mwanadamu na jini ina hukumu gani katika sheria ya kiislam?
( d ) Je kujamiiana kati ya mwanadamu na jini kuna ulazimu kuoga janaba?
( e ) Je watoto wanaotokana na majini na wanadamu wapo katika hali gani?
( f ) Nini hukumu ya mwanamke aliyetekwa mume wake na jini
( g ) Je majini wanakula na kunywa?
( h ) Wapi yapo makazi ya majini
( i ) Je wana vipando vya kupanda?
Hivyo basi tutaanza na dondoo ya mwanzo inayohusu ndoa za majini na kizazi chao. Ni kweli kwamba majini wanaoana na kuzaana na hilo limethibitishwa na kitabu chetu kitakatifu na sunna za Mtume Muhammad (SAW). Katika Quran Tukufu Allah (SWT) amesema: "Je! Mnamfanya yeye na kizazi chake kuwa marafiki ( zenu ) badala yangu, hali wao ni maadui zenu?" Al - Kahf 50. Aya hii inafahamisha wazi kwamba majini wanaoana kwa ajili ya kupata watoto, vile vile Allah (SWT) anatuambia katika sehemu nyingine katika Qur-an akituhadithia kuhusu wanawake wa peponi akisema: "watakuwepo huko wanawake watulizao macho yao, ambao hawajaingiliwa na binadamu wala majini katu." Ar-rahman 56. Aya hii pia inaonyesha kwamba majini nao huingiliana na kuziondoa bikira na kujamiiana. Ama upande wa sunnah za Mtume (SAW) zinazofahamisha ndoa zao na kuzaliana ni neno lake mtume (SAW) aliposema: "Hakika majini wanazaliana kama wanavyozaliana wanadamu, nao ni wengi mno idadi yao." Ameipokea hadithi hii Hatim na Abus-Sheikh- katika Al-Adhamah kutokana na Qataadah.
Je kuna ndoa kati ya majini na watu?
Imeenea katika baadhi ya maeneo kwamba kuna mtu ameoa jini; au kwamba mwanamke wa kibinadamu kaolewa na jini au ameposwa, kuna ukweli gani katika jambo hili? Ni kweli kwamba ndoa huenda ikawa kati ya mwanadamu na jini, Allah (SWT) anasema katika Qur-an Tukufu, "Nashirikiana nao katika mali ( zao ) na watoto ( wao )." Al - Israa 64. Akasema Mtume (SAW), "Anapokutana na mume na mkewe pasi na kutamka jina la Allah, basi shetani hushirikiana na huyo mume katika tendo la ndoa." Hadithi hii ameitoa Shubly katika kitabu Ahkamul - Murjaan. Na amepokea Hafidhi bin Jarir kutoka kwa Ibn Abbas (RA) kwamba Mtume (SAW) amesema: "Pindi amwingiliapo mume mkewe wakati akiwa katika hedhi, shetani humtangulia na ( mkewe ) akishika mimba basi atazaa mtoto ( khanithi ). Na ( makhanithi ) ni watoto wa majini." Na kuhusiana na hilo amesisitizia Ibn Taymiyah kwamba: "Inatokea kujamiiana kati ya majini na wanadamu na ikiwa ni hivyo basi huzaliwa watoto mara nyingi ( kwa kujamiiana huko ) kwa inavyofahamika." Wanazuoni wa mambo ya historia wameelezea kuhusu habari zilizotangulia zinazohusiana na ndoa kati ya majini na binadamu tutataja kisa kimojawapo, kisa kilichotolewa na Abu Bakar bin Abid-Dunia, kutokana na Abu Yusuf Saruji kwamba yeye amesema: "Alikuja mwanamke mmoja kwa bwana mmoja huko Madina, akamwambia: 'Hakika sisi tumeshukia hapa jirani je utanioa?' Basi yule bwana akamwoa, kisha baada ya muda yule jinni ( mke ) akamwambia yule bwana, 'umefika wakati wa kuondoka, basi naomba unipe talaka.' Na alikua akimjia usiku katika maumbile ya mwanamke. Ikatokea baada ya kumpa talaka akamwona siku moja katika mtaa mmoja ( jinni ) huyo akiokota nafaka zilizoanguka kutoka kwa wauzaji wa mazao. Akamwuliza ( jinni huyo ), 'Je unazihitaji nafaka hizi?' Yule jini akaweka mkono wake kichwani kuonyesha kuumbuka, kisha akainua uso wake akamtazama yule bwana, akamwuliza, 'umenionaje?' Yule bwana akajibu, 'kwa jicho hili', yule jini akanyoosha kidole chake kwenye lile jicho la yule bwana na kulipofua."
Na pamoja na kwamba kuna visa vingi vilivyopokewa kuhusu kuwepo ndoa kati ya wanadamu na majini, isipokua kuna wanaodai ya kwamba Majini wana asili ya maumbile ya moto, na wanadamu wana asili ya vitu vinne ( Hewa, maji, udongo na joto ), hivyo basi kuwepo kwa asili ya moto katika majini kunazuia kukaa yale ( manii ) ya binadamu katika tumbo la uzazi la jini, kutokana na moto uliopo.
Hivyo tutaelezea uwezekano huo katika toleo lijalo Inshaallah, usilikose.
WABILLAHI TAWFIQ
و بالله التوفيق