بسم الله الرحمن الرحيم
MAJINI
7
Masuala kuhusiana na ndoa kati ya Majini na watu, chakula cha Majini
Sheikh Mustafa Mohamed Kihago
MAJINI 1 | MAJINI 2 | MAJINI 3 | MAJINI 4 | MAJINI 5 | MAJINI 6 | MAJINI 7 | MAJINI 8 | MAJINI 9 |
Bonyeza hapa kusoma maudhui ya kila makala
Shukrani za dhati zimwendee Allah (SWT). Pia rehema na amani ziwe juu ya kipenzi chake Muhammad (SAW), pamoja na masahaba wake wote.
Imepokewa na Ahmad kutoka kwa Ubaid bin Umair kwamba Iblis alisema: "Ee Mola wangu, umenitoa mimi peponi kwa sababu ya Adam, na mimi sitomweza isipokua kwa nguvu za ufalme wako". Allah (SWT) akamwambia: "Basi tutakusalitisha nae. " Akasema: "Ee Mola wangu nizidishie." Akamwambia: "Basi hatopatikana mtoto wa kibinadamu isipokua atazaliwa na mtoto wako vile vile." Akasema: "Ee Mola wangu nizidishie." Akamwambia: "Vifua vyao vitakua ndio sehemu yako na utatembea katika mishipa yao ya damu." Na hiyo ni sawa na kauli ya Allah (SWT) katila Qur-an Tukufu aliposema: "Na uwakusanyie jeshi lako la wapandao farasi na waendao kwa miguu. Na shirikiana nao katika mali zao na watoto wao, na waahidi ahadi za uongo. Na shetani hana ahadi isipokua ni udanganyifu." Al - Israa 64.
Akasema Adam: "Ee Mola wangu umenisalitishia Iblisi na mimi sitoweza kujikinga nae isipokua kwako." Allah (SWT) akamwambia: "Kila mtoto atakayezaliwa kwako nitamwekea mlinzi wa kumlinda na mashetani wabaya." Akasema: "Ee Mola wangu nizidishie." Akamwambia: "Jema moja nitalipa mara kumi na zaidi, na baya nitalipa mara moja na ninaweza kulifuta." Akasema: "Ee Mola wangu nizidishie." Akamwambia: "Mlango wa toba sitaufunga kwa mja wangu akiwa bado yupo hai." Akasema: "Ee Mola wangu nizidishie." Akamwambia: "Ninasamehe makosa yote wala sijali." Hapo Adam akasema: "Imetosha." Allah (SWT) anasema: "Enyi waja wangu mliopindukia katika maovu msije mkaiacha rehema ya Allah (SWT). Hakika Allah (SWT) husamehe madhambi yote." Hivi ndivyo alivyo mwanadamu na shetani ambaye ni katika majini.
( a ) Je kujamiiana kati ya majini na wanadamu kuna wajibu wa mtu kuoga janaba?
Aliuliza swali hili Abul-Maaliy wa dhehebu la Hanbali, kwamba kuna mwanamke mmoja alisema: 'kuna jini anayenitokezea kama vile awavyo mume na mke, je? nawajibika kuoga janaba?' Hapo baadhi ya wafuasi wa Imam Hanbal walisema, 'huyo hatooga janaba.' Abu-Maaliy akasema: 'Hata kama huyo mwanamke angesema, 'ameniingilia mimi jinni kama vile mwanaume afanyavyo' pia halazimiki kuoga janaba, hiyo ni kutokana na kukosekana ushahidi wa kuingiliwa na kushusha, hivyo basi hali hiyo ni sawa na kuota ndoto.'
( b ) Nini hukumu ya mke aliyetoweka mumewe kwa kutekwa na jini?
Kisa kama hiki kilitokea wakati wa utawala wa Khalifa wa pili Umar bin Alkhatab (RA). Kuna bwana mmoja alikwenda kusali sala ya Isha akiwa na jamaa zake, akatoweka. Mke wake akenda kwa Umar bin Alkhatab (RA) akamwelezea kuhusu mume wake. Umar (RA) akawauliza jamaa zake kuhusu maelezo ya yule mwanamke, wakasema ni kweli mume wake katoweka. Hivyo Umar (RA) akamwamuru yule mwanamke angojee na kumsubiri mumewe kwa muda wa miaka minne. Yule mwanamke akafanya hivyo. Baada ya miaka minne kupita, akarudi tena kwa Sayyidna Umar (RA) akamwambia kwamba miaka minne imepita na hakuna dalili yeyote ya kuonekana mume wake. Sayyidna Umar (RA) akawauliza jamaa zake. Nao wakamwambia kuwa ni kweli bado hajatokea. Hivyo akampa ruhusa ya kuolewa. Alipoolewa tu, yule mume wake wa kwanza akatokea, ikabidi aende kwa Sayyidna Umar (RA) akamwambia: 'Mtu unatoweka bila ya jamaa zako kuwa na taarifa yeyote kuhusu wewe.' Yule bwana akamwambia nilikuwa nina udhuru, Sayyidna Umar (RA) akamuuliza: 'udhuru gani huo.' Yule bwana akasema, 'siku moja nilipokuwa nakwenda msikitini kusali sala ya Isha nilikumbwa na jinni mwanamke - Nikawekwa kwao muda mrefu. Wakavamiwa na majini waislam. Waliovamiwa wakashindwa vita na wengine kuuawa na wengine wakatekwa, nami nikawa ni katika mateka. Wakaniuliza kuhusu dini yangu. Nikawaambia kwamba mimi ni mwislam. Wakaniambia kwamba wao pia ni waislam, hivyo si halali kwao kunifanya mimi ni mateka. Hivyo wakaniambia nichague kati ya kuondoka kurejea kwetu au kukaa nao, ndipo nilipochagua kurejea kwetu. Wakawa wakinimulikia usiku kwa vijinga vya moto na mchana nikifuata mwelekeo wa upepo kurudi.' Umar (RA) akamuuliza, 'ulikuwa ukila nini?' Akasema: 'kila kilichokua hakitajwi jina la Mwenyezi Mungu ( yaani nyamafu ).' Akamuuliza tena, 'Nini ulikua ukinywa?' Akajibu: 'kila kilichokuwa kama mvinyo.' Hapo Umar (RA) akamwambia kwamba anaweza kumrudia mke wake au achukue mahari yake kutoka kwa yule mkewe.
(c) Ni kipi chakula cha majini?
Kuna tofauti nne kuhusu chakula chao: Kuna wanaosema kwamba majini hawali wala hawanywi, kuna wanaosema kwamba baadhi yao wanakula na kunywa na baadhi nyingine hawanywi wala hawali. Kuna wanaosema kwamba majini wote wanakula na kunywa na hii ndio rai sahihi kulingana na kitabu kitakatifu Qur-an na sunna za Mtume Muhammad (SAW) aliposema, "Shetani atakuwa anakula na mtu, mpaka atakapotaja jina la Allah (SWT), shetani atatapika kile alichokula tumboni." Na katika sehemu nyingine alisema, "Msiende haja kwa kutumia samadi au mifupa kwani hivyo ni vyakula vya ndugu zenu majini." Na katika sehemu nyingine anatukataza kula kwa mkono wa kushoto kwani yeye alisema, "Anapokula mmoja wenu atumie mkono wake wa kulia, na anapokunywa atumie vilevile mkono wake wa kulia, kwani shetani anakula na kunywa kwa kutumia mkono wa kushoto." Huo ni ushahidi wa kutosha wa kuonyesha kwamba majini wanakula na kunywa.
WABILLAHI TAWFIQ
و بالله التوفيق