بسم الله الرحمن الرحيم
MAJINI
3
Je Majini wana miili, majina, uwezo wa kujibadilisha, hufa? wanatembeaje? Muda gani wanatapanyika mashetani? Kiti cha enzi cha Iblis, mayoe ya Iblis na mambo aliyotangulia kufanya
Sheikh Mustafa Mohamed Kihago
MAJINI 1 | MAJINI 2 | MAJINI 3 | MAJINI 4 | MAJINI 5 | MAJINI 6 | MAJINI 7 | MAJINI 8 | MAJINI 9 |
Bonyeza hapa kusoma maudhui ya kila makala
Shukrani za dhati zimwendee Allah (SWT). Pia rehema na amani ziwe juu ya kipenzi chake Muhammad (SAW), pamoja na masahaba zake wote.
Majini ni viumbe wa Allah (SWT) ambao wanaonekana na kufahamika kimakosa na wengi kati yetu. Hii ni kutokana na kuwa wao wanatuona lakini sisi hatuwaoni.
1. Je majini wana miili?
Kwa wale wenye ujuzi na elimu ya maisha yao wametofautiana katika pande mbili kwa kauli mbili tofauti.
Kundi la mwanzo limeonelea kwamba hawa viumbe majini hawana maumbile kama tunavyofahamu miili ilivyo, bali ni mada iliyopo katika hali aliyoiumba Allah (SWT).
Kundi la pili linaonelea kwamba majini wana maumbile ya aina fulani fulani na wenye kauli hii nao wametofautiana. Kuna wanaosema kwamba maumbile yao ni kama kioo, 'transparent' ( ambapo ukiangalia unaweza kuona upande wa pili ), au ni maumbile yanayobadilika kuchukua sura mbali mbali na vile vile yawezekana pia kuwa wapo katika hali kama ya hewa ( hewani ).
Na kuna waliosema kwamba miili yao ni laini 'soft' mno kiasi kwamba si rahisi kuonekana na macho yetu, kutokana na udhaifu wa kuona tuliokua nao. Kwani Allah (SWT) angeweza kutupa uwezo wa kuwaona tungeliwaona. Na kile kinachofahamisha ulaini wa maumbile yao ni ushahidi uliopo katika Qur-an Tukufu katika neno lake Allah (SWT) aliposema: "Hakika yeye ( shetani ) pamoja na kabila lake wanakuoneni, hali ya kuwa ninyi hamwaoni", Al-A'raaf 27. Haya ni baadhi ya maoni na ushahidi uliopokelewa. Hivyo sote tunatosheka na ushahidi kwamba macho yetu hayakupewa uwezo wa kuwaona, lakini wao wanatuona.
2. Je majini wana majina mengine?
Jawabu ni ndio; majini wana majina mbali mbali katika lugha ya kiarabu tutataja baadhi yake:
( a ) Jinni : Anapokusudiwa jinni tu. Na maana ya neno jinni ni kitu kisichoonekana au kilichofichika.
( b ) Aamir : Anapokusudiwa yule anaishi katika majumba ya watu.
( c ) Shetani : Anapokuwa na shari
( d ) Rauhaan : Yule anaewatokezea watoto
( e ) Afriit : Anapokuwa na nguvu za kupindukia
3. Je majini wana uwezo wa kujibadilisha?
Majini wana uwezo huo, tena uwezo mkubwa mno wa kujigeuza katika maumbile tofauti kama vile kuwa kama majoka, nge, farasi, ng'ombe, ngamia, kondoo na ndege. Na pia wana uwezo wa kujigeuza katika maumbile va kibinadamu.
4. Uwezo wa majini
Majini wana uwezo na nguvu ambazo ni zaidi ya alizonazo binadamu na miongoni mwa nguvu zao hizo ni ule uwezo wao mkubwa wa kusafiri. Na mfano wa haraka haraka ambao tungependa kuutoa ni ule wa ahadi ya mmoja kati ya Majini wenye nguvu, Afriit, alipomwahidi Nabii Suleyman (AS) katika baraza lake, kwamba angeweza kumletea kiti cha enzi cha Malkia wa Yemen kutoka huko mpaka pale walipo ambapo ni Palestina kabla ya Nabii Suleyman (AS) kuvunja kikao chake. Allah (SWT) anatuhadithia katika suratun - Naml aya ya 38, 39: "( Suleyman akakusanya mawaziri wake akasema): 'Enyi wakuu! Ni nani atakayeniletea kiti chake cha enzi kabla hawajakuja kwangu, hali ya kuwa wamekwisha silimu?' Mjasiri mmoja wa majini akasema: 'Mimi nitakuletea kabla hujainuka mahali pako hapo na mimi hakika ninazo nguvu na uwezo wa hilo na ni mwaminifu'". Miongoni mwa nguvu zao pia ni ule uwezo wa kupaa mbali mbinguni kusikiliza habari. Na hiyo ilikuwa kabla ya kuja Mtume Muhammad (SAW).
5. Je majini hufa?
Hilo halina shaka kwani nao wanajumuishwa kwenye tamko la Allah (SWT) katika Qur-an, suratur- Rahman 26, 27: " Kila kilichoko juu yake ( ardhi na mbingu ) kitatoweka; na inabaki dhati ya Mola wako ( tu Mwenyewe ) Mwenye utukufu na heshima ". Na Mtume (SAW) amesema katika dua: "Najilinda kwa utukufu wako, ambapo hapana mwingine apasaye kuabudiwa kwa haki isipokua wewe ambaye hufi, lakini majini na watu wote wanakufa", imepokewa na Bukhari. Hivyo, kutokana na ushahidi uliotangulia majini hufa kama wanavyokufa viumbe wengine lakini Iblisi yeye amepewa muda mrefu wa kuishi mpaka siku ya kiyama, kama inavyoeleza Qur-an Tukufu, Al-A'raaf 14, 15: "Akasema ( Shetani ), 'Nipe muda ( nisife ) mpaka siku watakapofufuliwa ( viumbe )'. Akasema( Allah SWT ), 'utakua ni miongoni mwa waliopewa muda ( lakini si mpaka wakati ulioutaja ).'"
6. Ni vipi wanavyotembea mashetani?
Katika hili Mtume (SAW) anatufundisha kwa kusema: "Yeyote kati yetu asitembee na kiatu kimoja kwani shetani hutembea na kiatu kimoja."
7. Ni muda gani ambao wanatapanyika mashetani?
Wanatapanyika wakati unapoingia usiku na hiyo ni kutokana na uthibitisho wa hadithi ya Mtume (SAW) aliposema, "Unapoingia usiku au linapoingia giza wazuieni watoto wenu ndani, kwani mashetani hutapanyika wakati huo, litakapopita lisaa limoja baadaye muachilie, na fungeni milango na mumtaje Allah (SWT), kwani hakika shetani hafungui mlango uliofungwa." Imepokewa na Bukhari kutokana na Jabir bin Abdallah.
8. Wapi kipo kiti cha enzi cha Iblis?
Kiti cha enzi cha Iblis kipo baharini. Imepokewa na Imam Ahmad kutoka kwa Jabir kwamba Mtume (SAW) amesema, "Hakika Iblisi ameweka kiti chake cha enzi kwenye maji, kisha hutuma majeshi yake."
9. Mayoe ya Iblisi
Ametoa mayoe Iblisi mara nne:
( a ) Kapiga yoe wakati alipolaaniwa
( b ) Wakati alipotolewa kwenye pepo
( c ) Wakati alipopewa utume Mtume Muhammad (SAW)
( d ) Wakati ilipoteremshwa Suratul - Fatihah
10. Mambo aliyotangulia kufanya Iblisi kabla ya binadamu
( a )Iblisi ndiye aliyetangulia kulia kwa sauti
( b )Iblisi ndiye aliyetangulia kulinganisha ubora wa viumbe, yaani yeye ndiye wa mwanzo kujilinganisha na mwanadamu na kujiona bora.
( c )Naye ndiye aliyeanzisha nyimbo na kuimba
Tukutane katika toleo lijalo linalohusu: Je Iblisi alikuwa ni miongoni mwa majini au alikuwa ni Malaika?
WABILLAHI TAWFIQ
و بالله التوفيق